Nagona
Paperpack

Nagona ni riwaya fupi ya kifalsafa na kibaadausasa inayoibua fikra juu ya falsafa na maana ya uhai, maisha, dhamiri na hata fikra yenyewe. Mhusika kiini wa novela hii anajikuta katika mazingira ya ajabuajabu katika nyakati tofauti tofauti. Si rahisi kubaini iwapo ni maono, njozi, fikra ama matendo halisi, pengine ni vyote kwa pamoja. Unachoweza kubaini ni kuwa, katika hali zote hizi, yu akidadisi ama safarini kusaka jambo fulani. Katika safari yake hii anakutana na wahusika tofauti na wenye sifa za ajabuajabu. Wahusika hawa, wanaonekana kufurahi kumuona na wanabainisha kuwa yeye pekee ndiye waliyekuwa wakimsubiri muda wote na ndiye tegemeo lao. Yumkini yeye ndiye mkombozi wa pili. Hivyo, wanajiunga naye na safari inaendelea, ila fumbo linabaki, ukombozi gani anapaswa kuleta? Dhidi ya nini? Na, kwa vipi? Je, itakuwa lini? Hivi vinabaki kuwa ni vitendawili vya kifalsafa. Katika matukio yote haya, ambayo mengi hayasawiri moja kwa moja uhalisia wa duniani bali kuwa katikati ya fikra ama imani na uhalisi, muda unakwenda kwa kasi kubwa na inaonekana wazi kuwa ulimwengu upo katika changamoto za kiutawala, kifalsafa na hata kiimani. Katika mirengo yote hii, kinachotamalaki ni kukandamizwa kwa fikra na dhamiri, kushamiri kwa uongo dhidi ya ukweli, kificho dhidi ya uwazi na hata giza dhidi ya mwanga. Kila lililozoeleka linaonekana kuwa kikwazo dhidi ya ukweli ama usahihi ambao hauonekani licha ya kuwa bayana. Hali hii imetamalaki kiasi cha kusababisha hofu, vifo, kutofikiri na mikwamo katika mambo yote. Katika safari yake, mhusika kiini anakutana na wahusika waliowahi kufanya safari ya ukombozi ila wote wanakiri kuwa walikwamishwa na wanadamu na sasa mhusika kiini ndiye anayetarajiwa. 

Euphrase Kezilahabi

Euphrase Kezilahabi alizaliwa Namagondo, Ukerewe, Tanzania, tarehe 13/4/1944. Alisomea katika seminari ya Nyegezi, Mwanza (1957-66) na baadaye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikohitimu mwaka 1970. Alihitimu digrii ya Uzamivu katika Fasihi katika Chuo Kikuu cha Wisconsin, Madison, Marekani, mwaka 1985. Alikuwa Mhadhiri na baadaye Profesa Mshiriki katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Chuo Kikuu cha Botswana hadi alipougua mwaka 2019. Kezilahabi alifariki tarehe 9/1/2020 na kuzikwa, Namagondo, Ukerewe tarehe 13/1/2020. Mbali na DHIFA, Kezilahabi ameandika vitabu vingine 9, zikiwamo riwaya 6, tamthiliya 1 na diwani 2 za ushairi. Ameandika pia hadithi fupi nyingi.

This book is categorised in
Community Reviews
Related Books
Book Details
  • ISBN : 9789976587081
  • Publication Date : January 2023
  • Language : Swahili
  • Number of Pages : 111
  • Cover Format : Paperpack
  • Edition : Third Edition