Mzingile
Paperback

Mzingile ni novela (riwaya fupi) ya kifalsafa na kibaadausasa iliyochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1991. Riwaya hii ni pacha ya ile ya Nagona (1990). Riwaya hii inasawiri chimbuko, maendeleo, maangamizi na kuzaliwa upya kwa dunia kutokana na fujo za wanadamu. Kakulu, mhusika kiini wa novela hii, anasemekana kuwa alizaliwa kiajabuajabu, na umbo lake na maisha yake kwa jumla yalikuwa ni ya kushangaza na kutatanisha, yakihusishwa na matukio ya ajabu na uwezo usio wa kawaida aliosadikiwa kuwa nao. Hatimaye Kakulu anajitenga na jamii na kwenda kuishi peke yake juu ya kilima, lakini watu hawamwachi kwa amani kama anavyotaka, bali wanaendelea kumfuata na kumsujudia na kumhusisha na mambo ambayo yeye anasema hahusiki nayo. Hata baada ya karne nyingi bado watu wanamwamini na kumsujudia. Kwa njia hii kisasili cha Kakulu kinaundwa na uvumi unageuka kuwa ukweli. Unapotokea msiba unaodhaniwa kumhusu, anatumwa mjumbe (Msimulizi) kwenda kumtafuta Kakulu kumwarifu juu ya msiba huo. Safari hiyo ya karne nyingi inageuka kuwa msako wa utambuzi na ufunuo, na kuishia katika amagedoni inayoifuta dunia kongwe na kuasisi dunia mpya iliyo nje ya duara la Kakulu. Hii ni hadithi ya kifalsafa inayosaili simulizikuu zinazotawala duniani, ikiwamo ile ya kuumbwa, kuanguka na kukombolewa kwa dunia. Riwaya hii inatuchochea kuyatazama kwa jicho jipya yale tuliyozoea kuyafikiria kuwa kweli isiyosailika, zikiwamo imani za dini, siasa na sayansi. Ni hadithi inayoifikisha riwaya ya Kiswahili katika kiwango cha juu cha tafakuri na sanaa. Inafaa kusomwa na kila binadamu anayejali asili na hatima ya ulimwengu huu na watu wake.

Euphrase Kezilahabi

Euphrase Kezilahabi alizaliwa Namagondo, Ukerewe, Tanzania, tarehe 13/4/1944. Alisomea katika seminari ya Nyegezi, Mwanza (1957-66) na baadaye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikohitimu mwaka 1970. Alihitimu digrii ya Uzamivu katika Fasihi katika Chuo Kikuu cha Wisconsin, Madison, Marekani, mwaka 1985. Alikuwa Mhadhiri na baadaye Profesa Mshiriki katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Chuo Kikuu cha Botswana hadi alipougua mwaka 2019. Kezilahabi alifariki tarehe 9/1/2020 na kuzikwa, Namagondo, Ukerewe tarehe 13/1/2020. Mbali na DHIFA, Kezilahabi ameandika vitabu vingine 9, zikiwamo riwaya 6, tamthiliya 1 na diwani 2 za ushairi. Ameandika pia hadithi fupi nyingi.

Taarifa za kitabu
  • ISBN : 9789976587067
  • Tarehe ya kuchapishwa : January 2023
  • Lugha : Swahili
  • Idadi ya kurasa : 126
  • Aina ya kava : Paperpack

Jamii ya kitabu hiki ni
Maoni kutoka kwa jamii